MIRADI YA TASAF INAVYOSAIDIA KUINUA UCHUMI WA WATU MASIKINI NCHINI.

Mratibu wa TASAF halmashauri ya wilaya ya Nzega Jovitha Kakulu akizungumza na baadhi wa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru kaya masikini kijiji cha Sigili.

Na Odace Rwimo,Nzega DC

LICHA ya TASAF kutoa fedha za kijikimu kwa familia masikini lakini pia familia hizo zimebuni mbinu mbadala ili kuweza kujikwamua toka kwenye wimbi hilo la umasikini.

Mratibu wa TASAF Halmashauri ya wilaya ya Nzega Jovitha Kakulu anafanya Ziara kutembelea wanufaika wote wa Tasaf kwa lengo la kutaka kujua fedha wanazopewa walengwa kama zinatimiza mahitaji yao sanjari na kutoa elimu ya namna bora ya kutumia fedha hizo.

Aidha katika ziara yake amekutana na wanufaika wa kata ya Sigili Halmashauri ya wilaya ya Nzega Mkoani Tabora ambapo ameshangazwa na baadhi ya wanufaika kujikwamua kwenye dimbwa la umasikini kwa kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo ufugaji na kilimo.

Jovitha aliseema baadhi ya wanufaika wameanza kujitambua  kwa kufanya shughuli  za maendeleo kwa kutumia fedha wanazopata kwa kuanzisha aidha ufagaji wa kuku,mbuzi na Ng’ombe huku wengine wakianzisha vikundi vya kukopeshana fedha hali ambayo itasaidia kuondoa wimbi la umasikini kwenye baadhi ya kaya.

Alisema wapo ambao bado fedha za mradi wa Tasaf  hazijawanufaisha zaidi ya kuzitumia kwa mahitaji ya kujikumu chakula na vitu vingine kama nguo kutokana na kutokujua aidha ni kitu gani wanaweza kufanya kutumia  fedha hizo katika kuendeleza mitaji yao.


Mnufaika wa mpango wa Kunusuru kaya masikini nchini, TASAF Rose Jikukila akionesha ng'ombe ambao amenunua kupitia fedha anazopata kila mwezi.

Alisema wanaendelea kutoa elimu kwa wanufaika wote ili kuhakikisha ifikapo 2025 angalau asilimia 89.9 iwe imeanzisha miradi ya kiuchumi na zile familia ambazo tayari zina miradi zianze ujenzi wa nyumba za kuishi ili kuondokana na hali mbaya za maisha walizonazo sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti walengwa wa Tasaf ambao tayari wameanza kunufaika na fedha hizo walisema kabla ya mapango wa Tasaf wa kunusuru kaya masikini walikuwa na maisha magumu ambayo walishindwa kupata mahitaji muhimu kama chakula na mavazi.

“Unajua mpango wa TASAF umesaidia familia nyingi mfano mzuri ni kwa upande wa familia yangu nilikuwa na maisha magumu kupita kaisi lakini tangu nimejiunga na mpango huu wa kunusuru kaya masikini maisha yangu yamebadilika kwani tayari nimejenga na kununua ng’ombe hivyo najiona kati ya watu wenye maisha mazuri sasa”alisema Rose Jikukila.

Alisema kupitia mpango huo wa kunusuru kaya masikini,familia nyingi ambazo zilikuwa na watoto wa shule wamewafungulia dunia nyingine na kuweza kutimiza ndoto za watoto wao jambo ambalo lilikuwa gumu hapo awali.

Jikikula alisema kuna wimbi kubwa la watoto ambao walikuwa wanakosa elimu kutokana na umasikini kwenye kaya zao lakini sasa hali imebadiliki kwani idadi ya watoto hao imepungua na wengine wanasoma mpaka kufika chuo kikuu.

Aidha lipongeza serikali ya awamu ya sita jinsi ambavyo inazidi kuboresha mpango huo wa kunusuru kaya masikini zaidi ikiwa ni kupatiwa malipo ya mkupuo wa miezi miwili jambo ambalo linawasaidia kupanga bajeti zao vizuri na kufanya maendeleo ndani ya familia zao.

wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini katika kijiji cha Sigili wakifuatilia kwa makini elimu juu ya uundaji wa vikundi na kuanzisha miradi ya maendeleo

Kwa upande wake Elizabeth Masanyiwa mkazi wa kijiji cha Iboja kata ya Sigili alisema mpango wa Kunusuru kaya Masikini nchini umesaidia watu wengi kuondoka na umasikini ulio kithili kwani wengi wao walishindwa kumdu hata gharama za maisha yao hali iliyokuwa inapelekea mpasuko ndani ya familia.

Afisa Mfuatilia wa TASAF halmashauri ya Wilaya ya Nzega Irene Shayo akitoa elimu kwa wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya masikini juu ya Umuhimu wa kuboresha taarifa za walengwa na faida zake kwa kila hatua ya maboresho.

“Unanjua kuna familia nyingi zimevunjika kufuatia umasikini ambapo wanaume wengi walikuwa wanaamua kutelekeleza familia zao na kuziacha kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha ,jambo hili sasa limeanza kupungua kwa kiwango kikubwa kwani baadhi ya familia hizo sasa zinanufaika na mpango huo”alisema Masanyiwa

Alisema kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini baadhi ya wanufaika wameanza kubuni miradi mbalimbali ambayo imekuwa ikiinuwa familia  zao ikiwa ni ufugaji kuku,Mbuzi,Ng’ombe na kuanzisha vikundi vya kuchangishana fedha yaani kukopeshana hali ambayo inabadili maisha yao kwa kiwango kikubwa.

Kwa upande wake Afisa mfuatiliaji Irene Shayo aliwataka walengwa wote wa TASAF kuhakiki taarifa zao ikiwa ni pamoja kuboresha taarifa hasa kwa wale wanaopata watoto wadogo kwa kuwandikisha ili kuwapatia haki zao za msingi.

Alisema itakuwa vizuri kama mtu ataboresha taarifa pale familia inapoongezeka hasa kwa kupata motto kwani wengi wao wamekuwa hawafanyi hivyo jambo linalowanyima watoto wanaozaliwa kwenye familia hizo kutokuwa sehemu ya walengwa wanaonufaika na Mpango wa Kunusuru kaya masikini.