TUKAI AWATAKA WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI KUTIMIZA WAJIBU WAO.


Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora Naitapwaki Tukai akiwa na Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Eng.Modest Apolinary na afisa Utumishi Juma Kulwa wakiskiliza maoni ya watendaji wa kata na vijiji.

NA ODACE RWIMO,NZEGA  DC.

MKUU wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora Naitapwaki Tukai amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji kutumiza wajibu wa kazi zao ili kuendana  na kasi ya Rais wa Jamuhuri ya Muugano wa Tanzania Rais Samia Suluhu  Hassan kwa kusimamia miradi ya maendeleo kwa weredi.

Tamko hilo amelitoa wakati akizungumza na watendaji wa Kata pamoja na Vijiji kutoka Halmashauri ya wilaya ya Nzega mkoani hapa kwenye ukumbi wa CCM ambapo alisema miradi mingi inakwama kwenye Kata kutokana na baadhi ya watendaji kutokushiriki ipasavyo.

Alisema baadhi ya watendaji wa Kata na Vijiji wanashindwa kusimamia miradi ambayo ipo kwenye maeneo yao jambo ambalo halivumilika hata kidogo ikiwa ni pamoja na kutatua kero zilzipo kwenye maeneo yao ya kazi.

“Haiwezekani mpaka kiongozi wa kitaifa akija kutembelea miradi ndio tunaanza kusikia kero kutoka kwa wananchi wakati kwenye Kata kuna Mtendaji,na kijiji pia kina Mtendaji wameshindwa nini kutatua kero hizo na kama zimewashinda kwanini hazijawasilishwa  kwa Mkurugenzi ama hata ofisi ya mkuu wa Wilaya”alihoji DC Tukai.


Watendaji wa Kata Na Vijiji Wakisikiliza hotuba ya Mkuu wa wilaya ya Nzega Naitapwaki Tukai hayupo Pichani.

Alisema atakuwa mtu wa mwisho kuendelea kuvumilia mtumishi ambaye ameshindwa kutimiza wajibu wake kwa kuwa analipwa mshahara kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na si vinginevyo huku akisisitiza maadili ya utumishi wa umma kwa kila mtumishi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Halmashuri ya Wilaya ya Nzega Eng.Modest Apolinary amewataka watendaji hao kushiriki vyema katika ukusanyaji wa mapato kwenye vyanzo vyote vilivyopo kwenye kata na vijiji ili kukidhi mahitaji ya bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Alisema haiwezekani kuendelea kuwa nyuma wakati tunavyo vyanzo vingi ambavyo havikusanywi huku watendaji wa Kata na Vijiji wakishindwa hata kukusanya mapato yaliyopo kwenye maeneo yao ya kazi.

“Sipo tayari kuendelea kulea watumishi ambao hawawezi kusaidia halmsahauri kutimiza wajibu wa kuwahudumia wananchi wake kwani kuna miradi mingi ambayo ipo Katani na hata kwenye Vijiji inayotakiwa kukamilishwa kwa kutumia  mapato ya ndani.



Mkurugenzi mtendaji halmashauri ya wilaya ya Nzega Eng.Modest Apolinary akiwaeleza watendaji juu wajibu wao katika kata na vijiji wanavyovihudumu.

Katika hatua  nyingine Eng.Apolinary amewataka watendaji hao kusimamia miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao kwani kuna miradi mingi haiendi sawa wakatti watendaji wapo na hawafanyi lolote katika kusimamia utekelezaji wake.

Alisema kuna miradi mingi ambayo imeshindwa kukamilika kwa wakati na miradi mingine imesimama ama kwa kumaliza  fedha zilizo tolewa na serikali wakati mwingine migogoro baina ya wasimamizi na mafundi hali inayochangia baadhi ya miradi kusimama na kuchelewa kumalizika kwa wakati uliopangwa.